Pages

Saturday, 31 August 2013

MAANDAMANO MAKUBWA UINGEREZA KUPINGA VITA DHIDI YA SYRIA

Leo jiji la London, Uingereza, limeshuhudia maandamano makubwa ya kupinga aina yoyote ya mashambulizi tarajiwa dhidi ya taifa la Syria. Maandamano hayo yaliyoitishwa na wanaharakati mbalimbali wa upinzani, asasi za kiraia na taasisi zisizo za kiserikali zinazolingania amani, yamefanyika leo mjini hapo, lengo kuu likiwa ni kupinga siasa za vita zinazofuatwa na Marekani na waitifaki wake, dhidi ya nchi nyingine za dunia hususan Syria.

Maandamano hayo yanayotajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni nchini humo, yamewashirikisha pia wabunge na shakhsia wakubwa wa vitengo vya utamaduni na sanaa nchini Uingereza, yakiwa yameanzia katika eneo la Temple lililopo katikati ya jiji la London na kuelekea ofisi ya bunge na kisha ofisi ya Waziri Mkuu David Cameron. Hayo yanajiri katika hali ambayo, siku ya Alkhamis iliyopita, bunge la nchi hiyo liliupigia kura ya hapana muswada uliokuwa umewasilishwa na Cameron, wa kushirikiana na Marekani katika vita dhidi ya Syria, na kuilazimisha serikali ya nchi hiyo, kutangaza kuwa, haitoshiriki kwa namna yoyote katika mshambulizi dhidi ya taifa hilo la Syria. 

Weledi wa masuala ya kisiasa wameitaja hatua ya kupingwa na bunge la Uingereza mpango uliokuwa umependekezwa na waziri mkuu huyo kuwa ni kufeli kukubwa ambako hakujawahi kutokea kwa karne kadhaa. Takwimu zinaonyesha kuwa, karibu asilimia 11 hadi 25 tu ya wakazi wote wa Uingereza, ndio wanaoafiki mpango wa kushiriki nchi hiyo katika vita dhidi ya Syria, huku iliosalia ikipinga vikali suala hilo. Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu wa Uingereza kupingwa na bunge kuhusiana na suala la kwenda vitani, tangu mwaka 1782.



No comments:

Post a Comment