Pages

Friday, 23 August 2013

IKHWANUL MUSLIMIN WAANZA KUANDAMANA TENA MISRI

Duru za habari nchini Misri, zinaarifu kuanza tena maandamano ya wafuasi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin, yaliyoitwa kwa jina la “Ijumaa ya Mashahidi” mbele ya msikiti wa Al-Azizu Billah mjini Cairo. Habari zinasema kuwa, baada ya sala ya Ijumaa wafuasi wa harakati hiyo, wamefanya maandamano hayo katika mitaa ya Az-Zaytun, mjini hapo. 

Hata hivyo kulitokea vurugu baada ya wafuasi wa Ikhwanul Muslimin kutoa nara dhidi ya jeshi na kupelekea baadhi ya waumini waliokuwa wakisali nao kutoa radiamali dhidi ya wanaharakati hao. Hii ni katika hali ambayo, vyanzo vya habari vya harakati hiyo, vimeelezea kujiri maandamano makubwa katika miji ya Maghagha, Hush Isa, Al-Waraq, Al-Marajul-Arab- Alexandria, Halawan, Al-Matwariyyah na mingineyo. Kwa mujibu wa habari hiyo, mamia kadhaa ya wafuasi wa Ikhwanul Muslimin wamefanya maandamano mbele ya msikiti wa Al-Istiqamah mjini Al-Giza huku wakiwa wamebeba picha za rais Muhammad Mursi aliyeondolewa madarakani. 

Leo jeshi la Misri, lilishadidisha doria katika maeneo nyeti, kufuatia wito uliotolewa na Ikhwanul Muslimin wa kutaka yafanyike maandamano makubwa baada ya sala ya Ijumaa. Maeneo yanayotajwa kuwa na ulinzi mkali wa jeshi hilo ni pamoja na vituo vyote vya treni ya kasi, vituo vya magari huku ulinzi ukishadidishwa zaidi katika ikulu ya Al-Ittihaadiyyah, Medani ya Tahrir na Rabia al-Adawiyyah. 

Wakati huo huo, duru nyingine za habari zinaripoti kufanyika mazungumzo kati ya viongozi wa Ikhwanul Muslimin na serikali ya sasa nchini humo. Habari zaidi zinasema kuwa, mazungumzo hayo yalifanyika jioni ya jana Alkhamisi kwa kuhudhuriwa na baadhi ya wapatanishi, viongozi wa Ikhwan na wa serikali ya mpito, lengo kuu likiwa ni kumaliza tofauti za kisiasa zinazoikabili nchi hiyo hivi sasa.



No comments:

Post a Comment